Biblia ya King James Version
Yohana, Sura ya 2:
- Siku ya tatu palikuwa na arusi huko Kana ya Galilaya; na mama yake Yesu alikuwapo.
- Naye Yesu alikuwa amealikwa arusini pamoja na wanafunzi wake.
- Divai ilipokwisha, mama yake Yesu akamwambia, Hawana divai.
- Yesu akamwambia, Mama, nina nini nawe? saa yangu bado haijafika.
- Mama yake akawaambia watumishi, Lo lote atakalowaambia, fanyeni.
- Na hapo palikuwa na mitungi sita ya mawe, kama desturi ya Wayahudi ya kutawadha, kila moja yapata kadiri mbili tatu.
- Yesu akawaambia, Ijazeni mitungi hiyo maji. Wakavijaza mpaka ukingo.
- Akawaambia, Sasa choteni mkampeleke mkuu wa karamu. Nao waliibeba.
- Mkuu wa karamu alipoyaonja yale maji yaliyofanywa kuwa divai, asijue ilikotoka, (lakini wale watumishi walioteka maji walijua), mkuu wa karamu akamwita bwana arusi.
- Akamwambia, Kila mtu kwanza huandaa divai iliyo njema; na watu wakishakunywa sana, ndipo iliyo mbaya zaidi; lakini wewe umeiweka divai nzuri hata sasa.
- Mwanzo huo wa ishara Yesu aliufanya huko Kana ya Galilaya, akaudhihirisha utukufu wake; na wanafunzi wake wakamwamini.
- Baada ya hayo alishuka mpaka Kapernaumu, yeye na mama yake na ndugu zake na wanafunzi wake; wakakaa huko siku si nyingi.
- Pasaka ya Wayahudi ilikuwa karibu, naye Yesu akapanda kwenda Yerusalemu.
- Akawakuta Hekaluni watu waliokuwa wakiuza ng’ombe, kondoo na njiwa, na wavunja fedha wameketi.
- Akafanya mjeledi wa kamba, akawatoa wote nje ya hekalu, na kondoo na ng’ombe; akazimwaga fedha za wenye kuvunja fedha, akazipindua meza;
- Akawaambia wale waliokuwa wakiuza njiwa, Ondoeni vitu hivi hapa; msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa nyumba ya biashara.
- Wanafunzi wake wakakumbuka ya kuwa imeandikwa, Wivu wa nyumba yako umenila.
- Basi Wayahudi wakajibu, wakamwambia, Unatuonyesha ishara gani, kwamba unafanya haya?
- Yesu akajibu, akawaambia, Livunjeni hekalu hili, nami katika siku tatu nitalisimamisha.
- Basi Wayahudi wakasema, Hekalu hili lilijengwa kwa muda wa miaka arobaini na sita, nawe utalisimamisha kwa siku tatu?
- Lakini yeye alinena habari za hekalu la mwili wake.
- Basi alipofufuka katika wafu, wanafunzi wake wakakumbuka kwamba alikuwa amesema hayo; wakaamini Maandiko Matakatifu na yale maneno ambayo Yesu alisema.
- Yesu alipokuwa Yerusalemu katika sikukuu ya Pasaka, watu wengi waliamini jina lake walipoziona ishara alizozifanya.
- Lakini Yesu hakujikabidhi kwao, kwa sababu aliwajua wote.
- Wala haikuwa na haja ya mtu kushuhudia juu ya mwanadamu, kwa maana yeye alijua yaliyomo ndani ya mtu.