Kitabu cha Yohana, Biblia ya Sauti Bila Malipo, Biblia ya King James Version katika Kiswahili

Biblia ya King James Version

Yohana, Sura ya 1:

  1. Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu.
  2. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu.
  3. Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika.
  4. Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima; na huo uzima ulikuwa nuru ya watu.
  5. Nayo nuru yang’aa gizani; wala giza halikuiweza.
  6. Palikuwa na mtu, ametumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohana.
  7. Huyo alikuja kwa ushuhuda, ili aishuhudie ile Nuru, watu wote wapate kuamini kwa yeye.
  8. Yeye hakuwa ile nuru, bali alikuja kushuhudia ile nuru.
  9. Hiyo ndiyo nuru halisi, ambayo huwaangazia kila mtu ajaye ulimwenguni.
  10. Alikuwako ulimwenguni, na kwa yeye ulimwengu uliumbwa, wala ulimwengu haukumtambua.
  11. Alikuja kwa walio wake, na walio wake hawakumpokea.
  12. Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake;
  13. Waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu.
  14. Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu, nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba, amejaa neema na kweli.
  15. Yohana alishuhudia habari zake, akapaza sauti yake akisema, Huyu ndiye niliyenena habari zake ya kwamba, Ajaye nyuma yangu mkuu kuliko mimi, kwa maana alikuwa kabla yangu.
  16. Na katika utimilifu wake sisi sote tumepokea, na neema juu ya neema.
  17. Kwa maana torati ilitolewa kwa mkono wa Musa, bali neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo.
  18. Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote, Mwana pekee aliye katika kifua cha Baba, huyu ndiye aliyemfunua.
  19. Na huu ndio ushuhuda wake Yohana, Wayahudi walipotuma makuhani na Walawi kutoka Yerusalemu ili wamwulize, Wewe u nani?
  20. Naye alikiri, wala hakukana; lakini alikiri, Mimi siye Kristo.
  21. Wakamwuliza, Je! Je, wewe ni Eliya? Akasema, Si mimi. Wewe ni nabii yule? Naye akajibu, La.
  22. Basi wakamwambia, Wewe ni nani? ili tupate kuwajibu wale waliotutuma. Unasema nini juu yako mwenyewe?
  23. Akasema, Mimi ni sauti ya mtu aliaye nyikani, Inyosheni njia ya Bwana, kama alivyosema nabii Isaya.
  24. Na wale waliotumwa walikuwa wa Mafarisayo.
  25. Wakamwuliza, wakamwambia, Mbona basi wabatiza, ikiwa wewe si Kristo, wala Eliya, wala yule nabii?
  26. Yohana akawajibu, akasema, Mimi nabatiza kwa maji;
  27. Yeye ndiye ajaye baada yangu, ambaye mimi sistahili hata kuilegeza gidamu ya kiatu chake.
  28. Mambo hayo yalifanyika huko Bethania, ng’ambo ya mto Yordani, mahali Yohana alipokuwa akibatiza.
  29. Siku ya pili yake akamwona Yesu anakuja kwake, akasema, Tazama, Mwana-Kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu.
  30. Huyu ndiye niliyenena habari zake ya kwamba, Baada yangu anakuja mtu ambaye amekuwa mbele yangu kwa maana alikuwa kabla yangu.
  31. Wala mimi sikumjua, lakini mimi nalikuja nikibatiza kwa maji ili adhihirishwe kwa Israeli.
  32. Naye Yohana alishuhudia akisema, Nilimwona Roho akishuka kama njiwa kutoka mbinguni, akakaa juu yake.
  33. Wala mimi sikumjua; lakini yeye aliyenituma kubatiza kwa maji, huyo aliniambia, Yule utakayemwona Roho akishuka na kukaa juu yake, huyo ndiye abatizaye kwa Roho Mtakatifu.
  34. Nami nimeona na kushuhudia ya kuwa huyu ndiye Mwana wa Mungu.
  35. Kesho yake tena Yohane alikuwa amesimama pamoja na wanafunzi wake wawili;
  36. Akamtazama Yesu akitembea, akasema, Tazama, Mwana-Kondoo wa Mungu!
  37. Wanafunzi wawili wakamsikia akisema, wakamfuata Yesu.
  38. Yesu akageuka, akawaona wanamfuata, akawauliza, Mnatafuta nini? Wakamwambia, Rabi, (yaani, Mwalimu), unakaa wapi?
  39. Akawaambia, Njoni mwone. Wakaenda, wakaona mahali alipokuwa anakaa, wakakaa naye siku hiyo, kwa maana ilikuwa yapata saa kumi.
  40. Andrea, nduguye Simoni Petro, alikuwa mmoja wa wale wawili waliomsikia Yohane akisema hivyo, wakamfuata Yesu.
  41. Huyo akampata kwanza Simoni, ndugu yake, akamwambia, Tumemwona Masihi (maana yake Kristo).
  42. Naye akamleta kwa Yesu. Naye Yesu akamtazama, akasema, Wewe ndiwe Simoni, mwana wa Yona;
  43. Kesho yake Yesu alitaka kutoka kwenda Galilaya, akamkuta Filipo, akamwambia, Nifuate.
  44. Filipo alikuwa mwenyeji wa Bethsaida, mji wa Andrea na Petro.
  45. Filipo akamkuta Nathanaeli, akamwambia, Tumemwona yeye ambaye Mose aliandika habari zake katika torati, na manabii, Yesu, mwana wa Yusufu, wa Nazareti.
  46. Nathanaeli akamwambia, Je! Filipo akamwambia, Njoo uone.
  47. Yesu akamwona Nathanaeli anakuja kwake, akasema juu yake, Tazama, Mwisraeli kweli kweli, hamna hila ndani yake.
  48. Nathanaeli akamwambia, Umepataje kunijua? Yesu akajibu, akamwambia, Kabla Filipo hajakuita, ulipokuwa chini ya mtini, nilikuona.
  49. Nathanaeli akajibu, akamwambia, Rabi, wewe ndiwe Mwana wa Mungu; wewe ndiwe Mfalme wa Israeli.
  50. Yesu akajibu, akamwambia, Kwa sababu nilikuambia, Nilikuona chini ya mtini, waamini? utaona mambo makuu kuliko haya.
  51. Akamwambia, Amin, amin, nawaambia, Mtaziona mbingu zimefunguka, na malaika wa Mungu wakipanda na kushuka juu ya Mwana wa Adamu.