Biblia ya King James Version
Ufunuo, Sura ya 3:
- Na kwa malaika wa kanisa lililoko Sardi andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye na hizo Roho saba za Mungu, na zile nyota saba; Nayajua matendo yako, ya kuwa una jina la kuwa hai, nawe umekufa.
- Uwe mwenye kukesha, ukaimarishe mambo yaliyosalia, yanayokaribia kufa;
- Kumbuka basi jinsi ulivyopokea na kusikia, na ushike sana, ukatubu. Basi, usipokesha, nitakuja kwako kama mwivi, wala hutajua ni saa gani nitakayokuja juu yako.
- Unao majina machache hata katika Sardi watu ambao hawakuyatia mavazi yao uchafu; nao watakwenda pamoja nami wakiwa wamevaa mavazi meupe, kwa maana wamestahili.
- Yeye ashindaye atavikwa mavazi meupe; wala sitalifuta jina lake katika kitabu cha uzima, bali nitalikiri jina lake mbele za Baba yangu, na mbele ya malaika zake.
- Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa.
- Na kwa malaika wa kanisa lililoko Filadelfia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye mtakatifu, aliye wa kweli, aliye na ufunguo wa Daudi, yeye afunguaye wala hapana afungaye; naye hufunga wala hapana afunguaye;
- Nayajua matendo yako; tazama, nimeweka mbele yako mlango uliofunguliwa, wala hapana awezaye kuufunga, kwa maana unazo nguvu kidogo, nawe umelishika neno langu, wala hukulikana jina langu.
- Tazama, nakupa watu wa sinagogi la Shetani, wasemao kwamba ni Wayahudi, nao sio, bali wasema uongo; tazama, nitawafanya waje kusujudu mbele ya miguu yako, na kujua ya kuwa mimi nimekupenda.
- Kwa kuwa umelishika neno la subira yangu, mimi nami nitakulinda, utoke katika saa ya kuharibiwa iliyo tayari kuujilia ulimwengu wote, kuwajaribu wakaao juu ya nchi.
- Tazama, naja upesi; shika sana ulicho nacho, asije mtu akaitwaa taji yako.
- Yeye ashindaye nitamfanya kuwa nguzo katika hekalu la Mungu wangu, wala hatatoka nje tena, nami nitaandika juu yake jina la Mungu wangu, na jina la mji wa Mungu wangu, ambao ni Yerusalemu mpya; ashukaye kutoka mbinguni kwa Mungu wangu, nami nitaandika juu yake jina langu jipya.
- Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa.
- Na kwa malaika wa kanisa la Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, shahidi mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu;
- Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto.
- Basi, kwa kuwa una uvuguvugu, wala hu baridi wala hu moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.
- Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi;
- Nakupa shauri ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri; na mavazi meupe, upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane; na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona.
- Wote niwapendao mimi nawakemea na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu.
- Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami.
- Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda, nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi.
- Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa.