Biblia ya King James Version

Ufunuo, Sura ya 2:

  1. Kwa malaika wa kanisa la Efeso andika; Haya ndiyo anenayo yeye azishikaye zile nyota saba katika mkono wake wa kuume, yeye aendaye katikati ya vile vinara saba vya dhahabu;
  2. Nayajua matendo yako, na taabu yako, na subira yako, na jinsi huwezi kustahimili wabaya;
  3. nawe umevumilia, na kuwa na subira, na kwa ajili ya jina langu umetaabika, wala hukuzimia.
  4. Lakini nina neno juu yako, ya kwamba umeuacha upendo wako wa kwanza.
  5. Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka, ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza; usipofanya hivyo, nitakuja kwako upesi, na kukiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu.
  6. Lakini unayo neno hili, kwamba unayachukia matendo ya Wanikolai, ambayo mimi nayachukia.
  7. Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa; Yeye ashindaye, nitampa kula matunda ya mti wa uzima, ulio katikati ya bustani ya Mungu.
  8. Na kwa malaika wa kanisa lililoko Smirna andika; Haya ndiyo anenayo yeye wa kwanza na wa mwisho, ambaye alikuwa amekufa, kisha akawa hai;
  9. Nayajua dhiki yako na umaskini wako, (lakini u tajiri) najua na matukano ya hao wasemao kuwa ni Wayahudi, nao sio, bali ni sinagogi la Shetani.
  10. Usiogope mateso yatakayokupata; tazama, Ibilisi atawatupa baadhi yenu gerezani ili mjaribiwe; nanyi mtakuwa na dhiki siku kumi; uwe mwaminifu hata kufa, nami nitakupa taji ya uzima.
  11. Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa; Yeye ashindaye hatadhurika na mauti ya pili.
  12. Na kwa malaika wa kanisa lililoko Pergamo andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye na upanga mkali, wenye makali kuwili;
  13. Nayajua matendo yako, na ukaapo, ndipo penye kiti cha enzi cha Shetani; nawe walishika sana jina langu, wala hukuikana imani yangu; .
  14. Lakini ninayo maneno machache juu yako, kwa kuwa unao huko watu washikao fundisho la Balaamu, yeye aliyemfundisha Balaki aweke kikwazo mbele ya wana wa Israeli, wavile vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na kuzini.
  15. Vivyo hivyo nawe unao watu wayashikao mafundisho ya Wanikolai, jambo ambalo mimi nalichukia.
  16. Tubu; au sivyo, nitakuja kwako upesi, na kupigana nao kwa upanga wa kinywa changu.
  17. Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa; Yeye ashindaye nitampa ile mana iliyofichwa, nami nitampa jiwe jeupe, na katika hilo jiwe limeandikwa jina jipya asilolijua mtu ila yeye alipokeaye.
  18. Na kwa malaika wa kanisa lililoko Thiatira andika; Haya ndiyo anenayo Mwana wa Mungu, ambaye macho yake ni kama mwali wa moto, na miguu yake kama shaba iliyosuguliwa;
  19. Nayajua matendo yako, na upendo, na huduma, na imani, na subira yako, na matendo yako; na wa mwisho kuwa wengi kuliko wa kwanza.
  20. Lakini nina neno juu yako, ya kwamba unamruhusu yule mwanamke Yezebeli, yeye ajiitaye nabii na kuwafundisha watumishi wangu na kuwapoteza, ili wazinzi na kula vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu.
  21. Nami nimempa nafasi atubu, na kuacha uzinzi wake; wala hakutubu.
  22. Tazama, nitamtupa kitandani, na hao wazinio pamoja naye katika dhiki kubwa, wasipotubu matendo yao.
  23. Na watoto wake nitawaua; na makanisa yote yatajua ya kuwa mimi ndiye avichunguzaye viuno na mioyo, nami nitampa kila mmoja wenu kwa kadiri ya matendo yake.
  24. Lakini nawaambieni ninyi, na wengine walioko Thiatira, ninyi nyote msio na mafundisho hayo, nao wayanenavyo mafumbo ya Shetani; sitaweka juu yenu mzigo mwingine wowote.
  25. Bali mlicho nacho kishikeni sana mpaka nitakapokuja.
  26. Na yeye ashindaye, na kuyashika matendo yangu hata mwisho, nitampa mamlaka juu ya mataifa;
  27. Naye atawachunga kwa fimbo ya chuma; kama vyombo vya mfinyanzi vitavunjwa vipande vipande; kama mimi nilivyopokea kwa Baba yangu.
  28. Nami nitampa nyota ya asubuhi.
  29. Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa.