Nao wakawaeleza yaliyotukia njiani, na jinsi walivyomjua katika kuumega mkate.
Walipokuwa wakisema hayo, Yesu mwenyewe akasimama katikati yao, akawaambia, Amani iwe kwenu.
Lakini wakashtuka na kuogopa, wakidhani wameona roho.
Akawaambia, Mbona mnafadhaika? na kwa nini mawazo yanazuka mioyoni mwenu?
Tazameni mikono yangu na miguu yangu, ya kuwa ni mimi mwenyewe: nishikeni, mwone; kwa maana roho haina nyama na mifupa, kama mnionavyo mimi kuwa nayo.
Naye alipokwisha kusema hayo, akawaonyesha mikono na miguu yake.
Na walipokuwa bado hawakusadiki kwa furaha, wakistaajabu, akawaambia, Mna chakula cho chote hapa?
Wakampa kipande cha samaki wa kuokwa, na sega la asali.
Akakitwaa, akala mbele yao.
Akawaambia, Haya ndiyo maneno niliyowaambia nilipokuwa nikali pamoja nanyi, ya kwamba ni lazima yatimizwe yote yaliyoandikwa katika torati ya Musa, na katika manabii, na katika zaburi. mimi.
Ndipo akazifungua akili zao, wapate kuelewa na maandiko.
Akawaambia, Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu;
na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanzia Yerusalemu.
Na ninyi ni mashahidi wa mambo haya.
Na tazama, nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mjini, hata mvikwe uwezo utokao juu.
Akawaongoza nje mpaka Bethania, akainua mikono yake, akawabariki.
Ikawa alipokuwa akiwabariki, alijitenga nao, akachukuliwa juu mbinguni.
Wakamsujudia, wakarudi Yerusalemu wakiwa na furaha kuu.
wakawa daima ndani ya hekalu, wakimsifu Mungu. Amina.