Biblia ya King James Version
Yohana, Sura ya 15:
- Mimi ndimi mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima.
- Kila tawi ndani yangu lisilozaa huliondoa; na kila tawi lizaalo hulisafisha, ili lizidi kuzaa.
- Sasa ninyi mmekuwa safi kwa sababu ya lile neno nililowaambia.
- Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; hamwezi tena, msipokaa ndani yangu.
- Mimi ni mzabibu, ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote.
- Mtu asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka; na watu huyakusanya na kuyatupa motoni yakateketea.
- Ninyi mkikaa ndani yangu na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa.
- Hivyo hutukuzwa Baba yangu, kwa vile mzaavyo sana; nanyi mtakuwa wanafunzi wangu.
- Kama vile Baba alivyonipenda mimi, nami nilivyowapenda ninyi; kaeni katika pendo langu.
- Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake.
- Hayo nimewaambia, ili furaha yangu ikae ndani yenu, na furaha yenu ikamilike.
- Amri yangu ndiyo hii, Mpendane kama nilivyowapenda ninyi.
- Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.
- Ninyi ni rafiki zangu mkitenda ninayowaamuru.
- Tangu sasa siwaitii watumwa; kwa maana mtumwa hajui afanyalo bwana wake; kwa maana yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewajulisha.
- Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda, na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni.
- Haya ninayowaamuru ninyi mpendane.
- Kama ulimwengu ukiwachukia ninyi, mwajua kwamba umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi.
- Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda walio wake; lakini kwa kuwa ninyi si wa ulimwengu, bali mimi niliwachagua katika ulimwengu, kwa sababu hiyo ulimwengu unawachukia.
- Kumbukeni lile neno nililowaambia, Mtumwa si mkuu kuliko bwana wake. Ikiwa wameniudhi mimi, watawaudhi ninyi pia; ikiwa wamelishika neno langu, watalishika lenu pia.
- Lakini haya yote watawatenda ninyi kwa ajili ya jina langu, kwa sababu hawamjui yeye aliyenituma.
- Kama nisingalikuja na kusema nao, wasingalikuwa na dhambi; lakini sasa hawana la kujificha kwa dhambi yao.
- Anayenichukia mimi humchukia na Baba yangu pia.
- Kama nisingalifanya kati yao kazi asizozifanya mtu mwingine, wasingalikuwa na dhambi; lakini sasa wameniona na kunichukia mimi na Baba yangu pia.
- Lakini hii hutukia ili neno lililoandikwa katika torati yao litimie, Walinichukia bila sababu.
- Lakini ajapo huyo Msaidizi, nitakayewapelekea kutoka kwa Baba, huyo Roho wa kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia.
- Na ninyi pia mtashuhudia, kwa sababu mmekuwa pamoja nami tangu mwanzo.