Biblia ya King James Version

Yohana, Sura ya 14:

  1. Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi.
  2. Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia. naenda kuwaandalia mahali.
  3. Nami nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo.
  4. Na mimi niendako mwajua, na njia mnaijua.
  5. Tomaso akamwambia, Bwana, sisi hatujui uendako; na jinsi gani tunaweza kujua njia?
  6. Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.
  7. Kama mngalinijua mimi, mngalimjua na Baba yangu;
  8. Filipo akamwambia, Bwana, tuonyeshe Baba, na yatutosha.
  9. Yesu akamwambia, Mimi nimekuwa pamoja nanyi siku hizi zote, wewe usinijue, Filipo? yeye aliyeniona mimi amemwona Baba; nawe wasemaje basi, Utuonyeshe Baba?
  10. Husadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu? Maneno niwaambiayo mimi siyasemi kwa nafsi yangu;
  11. Mnisadiki ya kuwa mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu;
  12. Amin, amin, nawaambia, Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi yeye naye atazifanya; na kubwa kuliko hizo atafanya; kwa sababu mimi naenda kwa Baba yangu.
  13. Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana.
  14. Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya.
  15. Mkinipenda, mtazishika amri zangu.
  16. Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele;
  17. Hata Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa sababu haumwoni wala haumtambui; kwa maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu.
  18. Sitawaacha ninyi yatima, nitakuja kwenu.
  19. Bado kitambo kidogo na ulimwengu hautaniona tena; lakini ninyi mnaniona, kwa kuwa mimi ni hai, ninyi nanyi mtakuwa hai.
  20. Siku ile mtajua ya kuwa mimi niko ndani ya Baba yangu, nanyi ndani yangu, nami ndani yenu.
  21. Yeye aliye na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye; naye anipendaye atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda na kujidhihirisha kwake.
  22. Yuda, siye Iskarioti, akamwambia, Bwana, imekuwaje ya kwamba wataka kujidhihirisha kwetu, wala si kwa ulimwengu?
  23. Yesu akajibu, akamwambia, Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda, nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake.
  24. Yeye asiyenipenda, yeye hayashiki maneno yangu, na neno hilo mnalolisikia si langu, bali ni la Baba aliyenituma.
  25. Hayo nimewaambia nikiwa bado nipo pamoja nanyi.
  26. Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.
  27. Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi si kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiogope.
  28. Mmesikia jinsi nilivyowaambia, naenda zangu, tena naja kwenu. Kama mngalinipenda, mngalifurahi kwa sababu nimesema, naenda kwa Baba, kwa maana Baba yangu ni mkuu kuliko mimi.
  29. Na sasa nimewaambia kabla halijatokea, ili litakapotokea mpate kuamini.
  30. Sitasema nanyi maneno mengi baadaye, kwa maana yuaja mkuu wa ulimwengu huu, wala hana kitu kwangu.
  31. Lakini ili ulimwengu ujue kwamba nampenda Baba; na kama vile Baba alivyoniamuru, ndivyo nifanyavyo. Ondokeni, twende zetu.