Kitabu cha Yohana, Biblia ya Sauti Bila Malipo, Biblia ya King James Version katika Kiswahili
Biblia ya King James Version
Yohana, Sura ya 10:
Amin, amin, nawaambia, Yeye asiyeingia mlangoni katika zizi la kondoo, bali akwea na njia nyingine, huyo ni mwivi na mnyang’anyi.
Bali yeye aingiaye kwa mlango ndiye mchungaji wa kondoo.
Bawabu humfungulia yeye; na kondoo huisikia sauti yake, naye huwaita kondoo wake kwa majina, na kuwaongoza nje.
Naye awatoapo nje kondoo wake mwenyewe, huwatangulia, na kondoo humfuata, kwa maana waijua sauti yake.
Wala mgeni hawatamfuata, bali watamkimbia; kwa maana hawaijui sauti ya wageni.
Yesu aliwaambia mfano huo, lakini wao hawakuelewa aliyokuwa akiwaambia.
Basi Yesu akawaambia tena, Amin, amin, nawaambia, Mimi ndimi mlango wa kondoo.
Wote walionitangulia ni wezi na wanyang’anyi, lakini kondoo hawakuwasikia.
Mimi ndimi mlango; mtu akiingia kwa mimi, ataokoka, ataingia na kutoka, na kupata malisho.
Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele.
Mimi ndimi mchungaji mwema: mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo.
Lakini mtu wa mshahara, wala si mchungaji, ambaye kondoo si mali yake, humwona mbwa-mwitu anakuja, akawaacha kondoo na kukimbia, na mbwa-mwitu huwakamata na kuwatawanya.
Mtu wa mshahara hukimbia kwa sababu ni mtu wa mshahara, wala hajali kwa ajili ya kondoo.
Kama vile Baba anijuavyo mimi, nami nimjuavyo Baba; nami nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo.
Na kondoo wengine ninao, ambao si wa zizi hili; hao nao imenipasa kuwaleta, na sauti yangu wataisikia; na kutakuwa na zizi moja na mchungaji mmoja.
Kwa hiyo Baba anipenda, kwa sababu nautoa uhai wangu ili niutwae tena.
Hakuna mtu anayeninyang’anya, bali mimi nautoa kwa nafsi yangu. Ninao uwezo wa kuutoa, na ninao uwezo wa kuutwaa tena. Agizo hili nalipokea kwa Baba yangu.
Kukawa tena na mafarakano kati ya Wayahudi kwa ajili ya maneno hayo.
Wengi wao wakasema, Ana pepo, tena ana wazimu; mbona mnamsikia?
Wengine wakasema, Maneno haya si ya mwenye pepo. Je, shetani anaweza kufungua macho ya vipofu?
Na huko Yerusalemu kulikuwa na sikukuu ya kuweka wakfu, nayo ilikuwa ni majira ya baridi.
Naye Yesu alikuwa akitembea Hekaluni katika ukumbi wa Sulemani.
Basi Wayahudi wakamzunguka, wakamwambia, Je! utatutia shaka hata lini? Ikiwa wewe ndiwe Kristo, tuambie waziwazi.
Yesu akawajibu, “Niliwaambia, lakini hamkuamini; kazi nizifanyazo kwa jina la Baba yangu ndizo zinazonishuhudia.”
Lakini ninyi hamsadiki, kwa sababu ninyi si wa kondoo wangu, kama nilivyowaambia.