Biblia ya King James Version
Warumi, Sura ya 6:
- Tuseme nini basi? Tudumu katika dhambi ili neema izidi kuwa nyingi?
- Mungu apishe mbali. Sisi tulioifia dhambi tutaishije tena katika dhambi?
- Je! hamjui ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake?
- Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima.
- Kwa maana ikiwa tumeunganika katika mfano wa mauti yake, tutakuwa katika mfano wa kufufuka kwake.
- Tukijua neno hili, ya kuwa utu wetu wa kale ulisulubishwa pamoja naye, ili mwili wa dhambi uharibiwe, tusitumikie dhambi tena.
- Kwa maana yeye aliyekufa amewekwa huru mbali na dhambi.
- Basi ikiwa tumekufa pamoja na Kristo, tunaamini kwamba tutaishi pia pamoja naye.
- Tunajua kwamba Kristo, akiisha kufufuka katika wafu, hafi tena; kifo hakimtawali tena.
- Maana katika kufa kwake, aliifia dhambi mara moja tu; lakini kwa kuishi kwake, anamwishia Mungu.
- Vivyo hivyo ninyi nanyi jihesabuni kuwa wafu kwa dhambi, bali walio hai kwa Mungu katika Kristo Yesu.
- Basi, dhambi isitawale ndani ya miili yenu ipatikanayo na mauti, hata mkazitii tamaa zake.
- wala msitoe viungo vyenu kuwa silaha za dhuluma kwa dhambi; bali jitoeni wenyewe kwa Mungu kama walio hai baada ya kufa, na viungo vyenu kwa Mungu kuwa silaha za haki.
- Kwa maana dhambi haitawatawala ninyi, kwa maana hampo chini ya sheria, bali chini ya neema.
- Nini sasa? Tufanye dhambi kwa sababu hatuko chini ya sheria, bali chini ya neema? Mungu apishe mbali.
- Hamjui ya kuwa kwake yeye ambaye mnajitoa nafsi zenu kuwa watumwa wake katika kumtii, mmekuwa watumwa wake yule mnayemtii; kwamba ni utumishi wa dhambi uletao mauti, au utii uletao haki?
- Lakini Mungu na ashukuriwe kwa kuwa mlikuwa watumwa wa dhambi, lakini mmetii kwa mioyo yenu ile namna ya mafundisho mliyopewa.
- mlipokwisha kuwekwa huru mbali na dhambi, mkawa watumwa wa haki.
- Nanena kwa jinsi ya kibinadamu kwa sababu ya udhaifu wa miili yenu; vivyo hivyo sasa vitoeni viungo vyenu viwe watumishi wa haki hata utakatifu.
- Kwa maana mlipokuwa watumwa wa dhambi, mlikuwa huru mbali na uadilifu.
- Mlikuwa na matunda gani wakati ule kwa mambo yale ambayo mnayaonea haya sasa? maana mwisho wa mambo hayo ni mauti.
- Lakini sasa mkiisha kuwekwa huru mbali na dhambi, na kufanywa watumwa wa Mungu, mnayo matunda yenu ndiyo kutakaswa, na mwisho wake ni uzima wa milele.
- Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.