Biblia ya King James Version
Wakolosai, Sura ya 3:
- Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu.
- Yafikirini yaliyo juu, si yaliyo katika nchi.
- Kwa maana ninyi mmekufa, na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu.
- Kristo atakapotokea, aliye uhai wetu, ndipo ninyi nanyi mtakapotokea pamoja naye katika utukufu.
- Basi vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi; uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu;
- Kwa ajili ya mambo hayo huwajia ghadhabu ya Mungu wana wa uasi.
- ambayo ninyi nanyi mliziendea zamani mlipoishi ndani yake.
- Lakini sasa ninyi pia yawekeni haya yote; hasira, ghadhabu, uovu, matukano na matusi vinywani mwenu.
- Msiambiane uongo, kwa kuwa mmevua kabisa utu wa kale, pamoja na matendo yake;
- mkivaa utu mpya, unaofanywa upya upate ufahamu sawasawa na mfano wake yeye aliyeuumba;
- ambapo hakuna Myunani wala Myahudi, kutahiriwa wala kutokutahiriwa, mgeni wala Msikithe, mtumwa wala mtu huru; bali Kristo ni yote, na ndani ya yote.
- Basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu;
- mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama Kristo alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi.
- Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu.
- Na amani ya Mungu itawale mioyoni mwenu; ndiyo mliyoitiwa katika mwili mmoja; na kuweni wenye kushukuru.
- Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote; mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia Bwana kwa neema mioyoni mwenu.
- Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye.
- Enyi wake, watiini waume zenu, kama ipasavyo katika Bwana.
- Enyi waume, wapendeni wake zenu, wala msiwe na uchungu juu yao.
- Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika mambo yote, maana hilo lapendeza katika Bwana.
- Nanyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, wasije wakakata tamaa.
- Enyi watumwa, watiini mabwana zenu katika mambo yote; si kwa kuwatazama tu, kama wajipendezao; bali kwa unyofu wa moyo, mkimcha Mungu;
- Na lo lote mfanyalo, lifanyeni kwa moyo, kama kwa Bwana, wala si kwa wanadamu;
- mkijua ya kuwa mtapokea kwa Bwana ujira wa urithi; kwa kuwa mnamtumikia Bwana Kristo.
- Bali atendaye mabaya atapokea ubaya alioutenda; wala hakuna upendeleo.