Kitabu cha Wagalatia, Biblia ya Sauti Bila Malipo, Biblia ya King James Version katika Kiswahili
Biblia ya King James Version
Wagalatia, Sura ya 6:
Ndugu zangu, mtu akighafilika katika kosa lo lote, ninyi mlio wa Roho mrejezeni upya mtu kama huyo katika roho ya upole; ukijiangalia nafsi yako usije ukajaribiwa wewe mwenyewe.
Mchukuliane mizigo na kuitimiza hivyo sheria ya Kristo.
Maana mtu akijiona kuwa ni kitu, naye si kitu, anajidanganya nafsi yake.
Lakini kila mtu na aipime kazi yake mwenyewe, ndipo atakapokuwa na furaha katika nafsi yake peke yake, wala si kwa ajili ya mwingine.
Maana kila mtu atauchukua mzigo wake mwenyewe.
Yeye aliyefundishwa neno na amshirikishe yeye afundishaye katika mambo yote mema.
Msidanganyike; Mungu hadhihakiwi, kwa kuwa chochote apandacho mtu ndicho atakachovuna.
Maana yeye apandaye kwa mwili wake, katika mwili wake atavuna uharibifu; bali yeye apandaye kwa Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele.
Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho.
Kwa hiyo kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema, na hasa jamaa ya waaminio.
Mwaona jinsi herufi kubwa nilivyowaandikia kwa mkono wangu mwenyewe.
Wote wanaotaka kujionyesha kuwa wazuri kwa mwili, hao ndio huwashurutisha mtahiriwe; ila wasipate mateso kwa ajili ya msalaba wa Kristo.
Kwa maana hata wao wenyewe waliotahiriwa hawaishiki sheria; bali wanataka ninyi mtahiriwe, wapate kujivunia miili yenu.
Lakini mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu chochote isipokuwa msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu umesulubishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu.
Maana katika Kristo Yesu kutahiriwa si kitu, wala kutokutahiriwa, bali kiumbe kipya.
Na wote watakaoenenda kwa kanuni hiyo, amani na rehema iwe juu yao, na juu ya Israeli wa Mungu.
Tangu sasa mtu yeyote asinitaabishe, kwa maana ninachukua mwilini mwangu chapa za Bwana Yesu.
Ndugu, neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja na roho zenu. Amina.