Kitabu cha Waefeso, Biblia ya Sauti Bila Malipo, Biblia ya King James Version katika Kiswahili
Biblia ya King James Version
Waefeso, Sura ya 6:
Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana, maana hii ndiyo haki.
Waheshimu baba yako na mama yako; ambayo ndiyo amri ya kwanza yenye ahadi;
Upate heri, ukae siku nyingi katika nchi.
Nanyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, bali waleeni katika adabu na maonyo ya Bwana.
Enyi watumwa, watiini mabwana zenu kwa jinsi ya mwili kwa hofu na tetemeko, kwa unyofu wa mioyo yenu, kama kumtii Kristo;
si kwa kuwatazama tu, kama wapendezao watu; bali kama watumishi wa Kristo, mkitenda mapenzi ya Mungu kwa moyo;
mkitumikia kwa nia njema, kama kwa Bwana, na si kwa wanadamu;
mkijua ya kuwa kila neno jema alitendalo mtu atapokea hilo kwa Bwana, kwamba ni mtumwa au kwamba ni mtu huru.
Nanyi mabwana, wafanyieni vivyo hivyo, mkiacha kuwatisha, mkijua ya kuwa Bwana wenu naye yuko mbinguni; wala hakuna upendeleo kwake.
Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake.
Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za shetani.
Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama, bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.
Kwa hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.
Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani;
na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani;
zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu.
Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu;
kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;
Na kwa ajili yangu mimi, nipewe usemi, nifumbue kinywa changu kwa ujasiri, niihubiri ile siri ya Injili;
Kwa ajili ya hayo mimi ni mjumbe katika vifungo, ili nipate kunena kwa ujasiri kama inavyonipasa kunena.
Lakini ili ninyi nanyi mpate kujua mambo yangu, na jinsi ninavyoendelea, Tikiko, ndugu mpendwa na mtumishi mwaminifu katika Bwana, atawajulisha mambo yote.
ambaye nimemtuma kwenu kwa ajili hiyo, ili mpate kujua mambo yetu, na afariji mioyo yenu.
Amani na iwe kwa ndugu, na upendo pamoja na imani kutoka kwa Mungu Baba na kwa Bwana Yesu Kristo.
Neema na iwe pamoja na wote wampendao Bwana wetu Yesu Kristo kwa unyofu. Amina.