Biblia ya King James Version

Waefeso, Sura ya 2:

  1. Na ninyi mlikuwa wafu kwa sababu ya makosa na dhambi zenu;
  2. ambayo zamani mliziendea kwa kuifuata kawaida ya ulimwengu huu, kwa kumfuata mfalme wa uwezo wa anga, roho yule atendaye kazi sasa katika wana wa kuasi;
  3. ambao sisi sote tuliishi miongoni mwao zamani kwa kuzifuata tamaa za miili yetu, tukitimiza tamaa za mwili na nia; na kwa asili tulikuwa wana wa ghadhabu kama wengine.
  4. Lakini Mungu, ambaye ni mwingi wa rehema, kwa upendo wake mkuu aliotupenda.
  5. Hata tulipokuwa wafu kwa sababu ya dhambi zetu, alituhuisha pamoja na Kristo, (mmeokolewa kwa neema;)
  6. Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu;
  7. Ili katika nyakati zijazo audhihirishe wingi wa neema yake upitao kiasi kwa wema wake kwetu sisi katika Kristo Yesu.
  8. Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; wala hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu;
  9. wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu.
  10. Maana tu kazi yake, tuliumbwa katika Kristo Yesu, tutende matendo mema, ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili tuenende nayo.
  11. Kwa hiyo kumbukeni ya kwamba zamani ninyi mliokuwa Mataifa kwa jinsi ya mwili, mnaoitwa Wasiotahiriwa na wale waitwao, Waliotahiriwa katika mwili unaofanywa na mikono;
  12. Kwamba wakati ule mlikuwa hamna Kristo, mmefarakana na jumuiya ya Israeli, wageni wasio wa maagano ya ahadi.
  13. Lakini sasa, katika Kristo Yesu, ninyi ambao hapo kwanza mlikuwa mbali, mmekaribishwa kwa damu yake Kristo.
  14. Kwa maana yeye ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi sote tuliokuwa wawili kuwa mmoja, akakibomoa kiambaza cha kati kilichotutenga;
  15. akiisha kuuondoa ule uadui kwa mwili wake, yaani, ile sheria ya amri zilizo katika maagizo; ili kufanya hao wawili kuwa mtu mmoja mpya ndani yake, na kufanya amani;
  16. na ili kuwapatanisha wote wawili na Mungu katika mwili mmoja kwa njia ya msalaba, akiisha kuuua uadui kwa huo msalaba;
  17. Akaja akahubiri amani kwenu ninyi mliokuwa mbali, na kwa wale waliokuwa karibu.
  18. Maana kwa yeye sisi sote tumepata njia ya kumkaribia Baba katika Roho mmoja.
  19. Basi sasa ninyi si wageni wala wapitaji, bali ninyi ni wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa nyumbani mwake Mungu;
  20. Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni.
  21. Ambaye ndani yake jengo lote linaungamanishwa na kukua hata liwe hekalu takatifu katika Bwana.
  22. Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya Mungu katika Roho.