Biblia ya King James Version
Waefeso, Sura ya 2:
- Na ninyi mlikuwa wafu kwa sababu ya makosa na dhambi zenu;
- ambayo zamani mliziendea kwa kuifuata kawaida ya ulimwengu huu, kwa kumfuata mfalme wa uwezo wa anga, roho yule atendaye kazi sasa katika wana wa kuasi;
- ambao sisi sote tuliishi miongoni mwao zamani kwa kuzifuata tamaa za miili yetu, tukitimiza tamaa za mwili na nia; na kwa asili tulikuwa wana wa ghadhabu kama wengine.
- Lakini Mungu, ambaye ni mwingi wa rehema, kwa upendo wake mkuu aliotupenda.
- Hata tulipokuwa wafu kwa sababu ya dhambi zetu, alituhuisha pamoja na Kristo, (mmeokolewa kwa neema;)
- Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu;
- Ili katika nyakati zijazo audhihirishe wingi wa neema yake upitao kiasi kwa wema wake kwetu sisi katika Kristo Yesu.
- Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; wala hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu;
- wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu.
- Maana tu kazi yake, tuliumbwa katika Kristo Yesu, tutende matendo mema, ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili tuenende nayo.
- Kwa hiyo kumbukeni ya kwamba zamani ninyi mliokuwa Mataifa kwa jinsi ya mwili, mnaoitwa Wasiotahiriwa na wale waitwao, Waliotahiriwa katika mwili unaofanywa na mikono;
- Kwamba wakati ule mlikuwa hamna Kristo, mmefarakana na jumuiya ya Israeli, wageni wasio wa maagano ya ahadi.
- Lakini sasa, katika Kristo Yesu, ninyi ambao hapo kwanza mlikuwa mbali, mmekaribishwa kwa damu yake Kristo.
- Kwa maana yeye ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi sote tuliokuwa wawili kuwa mmoja, akakibomoa kiambaza cha kati kilichotutenga;
- akiisha kuuondoa ule uadui kwa mwili wake, yaani, ile sheria ya amri zilizo katika maagizo; ili kufanya hao wawili kuwa mtu mmoja mpya ndani yake, na kufanya amani;
- na ili kuwapatanisha wote wawili na Mungu katika mwili mmoja kwa njia ya msalaba, akiisha kuuua uadui kwa huo msalaba;
- Akaja akahubiri amani kwenu ninyi mliokuwa mbali, na kwa wale waliokuwa karibu.
- Maana kwa yeye sisi sote tumepata njia ya kumkaribia Baba katika Roho mmoja.
- Basi sasa ninyi si wageni wala wapitaji, bali ninyi ni wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa nyumbani mwake Mungu;
- Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni.
- Ambaye ndani yake jengo lote linaungamanishwa na kukua hata liwe hekalu takatifu katika Bwana.
- Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya Mungu katika Roho.