Biblia ya King James Version

Waebrania, Sura ya 10:

  1. Kwa maana torati, kwa kuwa ni kivuli cha mema yatakayokuwa, wala si sura yenyewe ya mambo hayo, kwa dhabihu zile wanazozitoa kila mwaka daima haziwezi wakati wo wote kuwakamilisha wakaribiao.
  2. Kwa maana hapo hangalikwisha kutolewa? kwa maana waabuduo, wakiisha kutakaswa mara moja tu, wasingekuwa na dhamiri ya dhambi tena.
  3. Lakini katika dhabihu hizo kuna ukumbusho wa dhambi kila mwaka.
  4. Kwa maana haiwezekani damu ya mafahali na mbuzi kuondoa dhambi.
  5. Kwa hiyo ajapo ulimwenguni, asema, Dhabihu na sadaka hukutaka, bali mwili umeniandalia;
  6. sadaka za kuteketezwa na dhabihu za dhambi hukupendezwa nazo.
  7. Ndipo nikasema, Tazama, nimekuja (katika gombo la chuo nimeandikiwa) niyafanye mapenzi yako, Ee Mungu.
  8. Hapo juu aliposema, Dhabihu na matoleo na sadaka za kuteketezwa na sadaka za dhambi hukutaka, wala hukupendezwa nazo; ambayo hutolewa na sheria;
  9. Ndipo akasema, Tazama, nimekuja kufanya mapenzi yako, Ee Mungu. Anaondoa la kwanza, ili alisimamishe la pili.
  10. Katika mapenzi hayo tumetakaswa kwa toleo la mwili wa Yesu Kristo mara moja tu.
  11. Na kila kuhani husimama kila siku akifanya ibada, na kutoa dhabihu zile zile mara nyingi, ambazo haziwezi kamwe kuondoa dhambi;
  12. Lakini huyu, alipokwisha kutoa dhabihu moja kwa ajili ya dhambi hata milele, aliketi mkono wa kuume wa Mungu;
  13. Tangu sasa akingoja hata adui zake wawekwe chini ya miguu yake.
  14. Maana kwa toleo moja amewakamilisha hata milele wale wanaotakaswa.
  15. Ambayo Roho Mtakatifu naye ni shahidi kwetu;
  16. Hili ndilo agano nitakaloagana nao baada ya siku zile, asema Bwana, nitatia sheria zangu mioyoni mwao, na katika nia zao nitaziandika;
  17. Na dhambi zao na maovu yao sitayakumbuka tena.
  18. Basi ondoleo la hayo likiwapo, hapana toleo tena kwa ajili ya dhambi.
  19. Basi, ndugu, kwa kuwa tuna ujasiri wa kupaingia patakatifu kwa damu ya Yesu;
  20. kwa njia mpya iliyo hai, aliyotuwekea, ipitayo katika pazia, yaani, mwili wake;
  21. tena tunaye kuhani mkuu juu ya nyumba ya Mungu;
  22. Na tukaribie wenye mioyo ya kweli, kwa utimilifu wa imani, hali tumenyunyiziwa mioyo tuache dhamiri mbaya, tumeoshwa miili kwa maji safi.
  23. Na tushike sana ungamo la imani yetu, bila kuyumba; (kwa maana yeye aliyeahidi ni mwaminifu;)
  24. Na tuangaliane sisi kwa sisi na kuhimizana katika upendo na matendo mema;
  25. wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia.
  26. Kwa maana kama tukifanya dhambi kusudi baada ya kuupokea ujuzi wa ile kweli, haibaki tena dhabihu kwa ajili ya dhambi;
  27. Bali kuna kuitazamia hukumu yenye kutisha na ukali wa moto utakaowala wao wapingao.
  28. Yeye aliyeidharau sheria ya Musa alikufa pasipo huruma kwa mashahidi wawili au watatu;
  29. Je! mnadhani atahesabiwa kuwa anastahili adhabu kali zaidi kiasi gani yeye aliyemkanyaga Mwana wa Mungu, na kuihesabu damu ya agano aliyotakaswa nayo kuwa ni kitu kisicho takatifu, na kumdharau Roho. ya neema?
  30. Maana twamjua yeye aliyesema, Kisasi ni juu yangu mimi, mimi nitalipa, asema Bwana. Na tena, Bwana atawahukumu watu wake.
  31. Ni jambo la kutisha kuanguka katika mikono ya Mungu aliye hai.
  32. Lakini zikumbukeni siku za kwanza, ambazo mlipokwisha kutiwa nuru, mlistahimili mashindano makubwa ya mateso;
  33. Pengine, mlipofanywa kuwa kitu cha kutazamwa kwa lawama na dhiki; na kwa sehemu mlipo kuwa washirika wa wale waliotumika hivyo.
  34. Kwa maana mlinionea huruma nikiwa vifungoni, mkakubali kwa furaha kunyang’anywa mali zenu, mkijua kwamba mnayo mali iliyo bora zaidi na idumuyo mbinguni.
  35. Basi msiutupe ujasiri wenu, ambao una malipo makubwa.
  36. Maana mnahitaji saburi, ili mkiisha kuyafanya mapenzi ya Mungu mpate ile ahadi.
  37. Kwa maana bado kitambo kidogo, na yeye ajaye atakuja, wala hatakawia.
  38. Basi mwenye haki ataishi kwa imani; lakini mtu akisita-sita, roho yangu haina furaha naye.
  39. Lakini sisi si miongoni mwao wanaorudi nyuma kwenye upotevu; bali wa wale wanaoamini kwa wokovu wa roho.