Biblia ya King James Version
Waebrania, Sura ya 1:
- Mungu ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi;
- Mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu;
- Yeye kwa kuwa ni mng’ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake, akivichukua vyote kwa neno la uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu;
- Amefanywa kuwa bora zaidi kuliko malaika, kwa vile alipata kwa urithi jina tukufu zaidi kuliko wao.
- Kwa maana alimwambia malaika yupi wakati wo wote, Wewe ndiwe Mwanangu, mimi leo nimekuzaa? Na tena, Nitakuwa kwake Baba, naye atakuwa kwangu Mwana?
- Na tena, amletapo mzaliwa wa kwanza ulimwenguni, asema, Na wamwabudu malaika wote wa Mungu.
- Na kuhusu malaika asema, Afanyaye malaika zake kuwa pepo, na watumishi wake kuwa miali ya moto.
- Lakini kuhusu Mwana asema, Kiti chako cha enzi, Mungu, ni cha milele na milele;
- Umependa haki, na kuchukia uovu; kwa hiyo Mungu, Mungu wako, amekupaka mafuta, Mafuta ya furaha kuliko wenzako.
- Na tena, Wewe, Bwana, hapo mwanzo uliiweka misingi ya nchi; na mbingu ni kazi za mikono yako;
- Wataangamia; lakini wewe unabaki; na zote zitachakaa kama vazi;
- Na kama vazi utazikunja, nazo zitabadilishwa; lakini wewe ni yeye yule, na miaka yako haitakoma.
- Lakini ni malaika yupi aliwahi kumwambia wakati wo wote, Uketi mkono wangu wa kuume, hata niwaweke adui zako chini ya miguu yako?
- Je! hao wote si roho watumikao, wakitumwa kuwahudumia wale watakaourithi wokovu?