Biblia ya King James Version
Ufunuo, Sura ya 13:
- Kisha nikasimama juu ya mchanga wa bahari, nikaona mnyama akitoka katika bahari, mwenye vichwa saba na pembe kumi, na juu ya pembe zake ana vilemba kumi, na juu ya vichwa vyake jina la makufuru.
- Na yule mnyama niliyemwona alikuwa kama chui, na miguu yake ilikuwa kama miguu ya dubu, na kinywa chake kama kinywa cha simba;
- Nikaona kimoja cha vichwa vyake kana kwamba kimetiwa jeraha la kufa; na jeraha lake la mauti likapona; ulimwengu wote ukastaajabia yule mnyama.
- Wakamsujudu yule joka kwa sababu alimpa huyo mnyama uwezo; ni nani awezaye kufanya vita naye?
- Naye akapewa kinywa cha kunena maneno makuu na ya makufuru; naye akapewa uwezo wa kufanya hivyo kwa muda wa miezi arobaini na miwili.
- Akafungua kinywa chake kumkufuru Mungu, na kulitukana jina lake, na maskani yake, nao wakaao mbinguni.
- Naye akapewa kufanya vita na watakatifu na kuwashinda, na akapewa uwezo juu ya kila kabila na lugha na taifa.
- Na wote wakaao juu ya nchi watamsujudu, ambaye jina lake halikuandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo, aliyechinjwa tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu.
- Mtu akiwa na sikio, na asikie.
- Anayeongoza utumwani atachukuliwa mateka, anayeua kwa upanga lazima atauawa kwa upanga. Hapa ndipo penye subira na imani ya watakatifu.
- Kisha nikaona mnyama mwingine, akipanda juu kutoka katika nchi; naye alikuwa na pembe mbili kama za mwana-kondoo, akanena kama joka.
- Naye atumia uwezo wote wa yule mnyama wa kwanza mbele yake, naye aifanya dunia na wote wakaao ndani yake kumwabudu yule mnyama wa kwanza, ambaye jeraha lake la mauti lilipona.
- Naye akafanya maajabu makubwa, hata kufanya moto kutoka mbinguni ushuke juu ya nchi mbele ya wanadamu;
- Naye akawadanganya wakaao juu ya nchi kwa ishara alizopewa kuzifanya mbele ya yule mnyama; akiwaambia wakaao juu ya nchi wamfanyie sanamu yule mnyama, aliyekuwa na jeraha la upanga, naye akaishi.
- Naye akapewa kutoa uhai kwa ile sanamu ya mnyama, hata ile sanamu ya mnyama inene, na kuwafanya wote wasioisujudia sanamu ya mnyama wauawe.
- Naye awafanya wote, wadogo kwa wakubwa, na matajiri kwa maskini, na walio huru kwa watumwa, watiwe chapa katika mkono wao wa kuume, au katika vipaji vya nyuso zao;
- tena kwamba mtu awaye yote asiweze kununua wala kuuza, isipokuwa ana chapa ile, jina la yule mnyama, au hesabu ya jina lake.
- Hapa kuna hekima. Yeye aliye na akili na aihesabu hesabu ya mnyama yule; na hesabu yake ni mia sita sitini na sita.