Kitabu cha Pili cha Petro, Biblia ya Sauti Bila Malipo, Biblia ya King James Version katika Kiswahili
Biblia ya King James Version
Petro wa 2, Sura ya 3:
Wapenzi, barua hii ya pili ninayowaandikia sasa; katika hayo mawili naziamsha nia zenu safi kwa kuwakumbusha;
mpate kuyakumbuka maneno yaliyonenwa zamani na manabii watakatifu, na ile amri tuliyopewa mitume wa Bwana na Mwokozi.
Mkijua neno hili kwanza ya kwamba siku za mwisho watakuja watu wenye kudhihaki, wafuatao tamaa zao wenyewe;
na kusema, Iko wapi ahadi ya kuja kwake? kwa maana tangu mababu walipolala, vitu vyote vinakaa kama vile tangu mwanzo wa kuumbwa.
Maana hawakujua neno hili, ya kwamba kwa neno la Mungu mbingu zilikuwepo zamani, na nchi ilisimama kutoka katika maji na ndani ya maji;
Kwa hayo ulimwengu wa wakati ule uligharikishwa na maji, ukaangamia;
Lakini mbingu za sasa na nchi zimewekwa akiba kwa moto kwa neno lilo hilo, zikilindwa hata siku ya hukumu na ya kuangamizwa kwa watu wasiomcha Mungu.
Lakini, wapenzi, msisahau neno hili moja, ya kwamba kwa Bwana siku moja ni kama miaka elfu, na miaka elfu ni kama siku moja.
Bwana hakawii kutimiza ahadi yake, kama watu wengine wanavyohesabu kukawia; bali huvumilia kwa ajili yetu, hapendi mtu ye yote apotee, bali wote wafikilie toba.
Lakini siku ya Bwana itakuja kama mwivi; katika siku hiyo mbingu zitatoweka kwa mshindo mkuu, na viumbe vya asili vitaunguzwa na kuyeyuka, na nchi na kazi zilizomo ndani yake zitateketea.
Basi kwa kuwa vitu hivi vyote vitafumuliwa, imewapasa ninyi kuwa watu wa namna gani katika mwenendo mtakatifu na utauwa?
Mkitazamia na kuharakisha kuja kwa siku ile ya Mungu, ambayo mbingu zitateketezwa kwa moto na kuharibiwa, na viumbe vya asili vitayeyushwa kwa joto kali?
Lakini sisi, kama alivyoahidi, tunatazamia mbingu mpya na dunia mpya, ambayo haki yakaa ndani yake.
Kwa hiyo, wapenzi, kwa kuwa mnatazamia mambo kama hayo, fanyeni bidii ili mpate kuonekana naye katika amani, bila mawaa wala lawama.
Na hesabuni uvumilivu wa Mola wetu kuwa ni wokovu; kama vile ndugu yetu mpenzi Paulo alivyowaandikia kwa hekima aliyopewa;
kama vile katika nyaraka zake zote, akinena ndani yake habari za mambo hayo; ambayo ndani yake yamo mambo mengine ni magumu kueleweka, ambayo watu wasio na elimu na wasio imara huyapotosha, kama wafanyavyo na maandiko mengine, kwa upotevu wao wenyewe.
Basi ninyi, wapenzi, mkitangulia kujua hayo, jihadharini, msije mkapotoshwa na makosa ya waovu, mkaanguka na kuuacha uthabiti wenu.
Lakini kueni katika neema na katika kumjua Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo. Utukufu una yeye sasa na hata milele. Amina.