Biblia ya King James Version
Mathayo, Sura ya 7:
- Msihukumu msije mkahukumiwa.
- Kwa maana hukumu ile mhukumuyo, ndiyo mtakayohukumiwa; na kipimo kile mpimacho, ndicho mtakachopimiwa.
- Na kwa nini wakitazama kibanzi kilicho katika jicho la ndugu yako, lakini huioni boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe?
- Au wawezaje kumwambia ndugu yako, Acha nikutoe kibanzi katika jicho lako; na tazama, boriti imo katika jicho lako mwenyewe?
- Mnafiki wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe; ndipo utakapoona vizuri kukitoa kile kibanzi katika jicho la ndugu yako.
- Msiwape mbwa kilicho kitakatifu, wala msiwatupe nguruwe lulu zenu, wasije wakazikanyaga chini ya miguu yao, wakageuka na kuwararua.
- Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtapata; bisheni, nanyi mtafunguliwa;
- Kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa.
- Au kuna mtu yupi kwenu ambaye mtoto wake akimwomba mkate, atampa jiwe?
- Au akimwomba samaki, atampa nyoka?
- Ikiwa ninyi, mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa mema wao wamwombao?
- Basi yo yote mtakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo; kwa maana hiyo ndiyo torati na manabii.
- Ingieni kwa mlango ulio mwembamba; maana mlango ni mpana, na njia ni pana iendayo upotevuni, nao ni wengi waingiao kwa mlango huo;
- Kwa maana mlango ni mwembamba, na njia imesonga iendayo uzimani, nao waionao ni wachache.
- Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali.
- Mtawatambua kwa matunda yao. Je! watu huchuma zabibu kwenye miiba, au tini kwenye michongoma?
- Vivyo hivyo kila mti mzuri huzaa matunda mazuri; bali mti mwovu huzaa matunda mabaya.
- Mti mzuri hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mbaya hauwezi kuzaa matunda mazuri.
- Kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni.
- Kwa hiyo kwa matunda yao mtawatambua.
- Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.
- Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako? na kwa jina lako kutoa pepo? na kwa jina lako kufanya miujiza mingi?
- Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi watenda maovu.
- Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba;
- Mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile; nayo haikuanguka, kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba.
- Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga;
- Mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile; ikaanguka: na anguko lake lilikuwa kubwa.
- Ikawa Yesu alipomaliza kusema hayo, umati wa watu ulishangazwa na mafundisho yake;
- Kwa maana aliwafundisha kama mtu mwenye mamlaka, wala si kama waandishi.