Biblia ya King James Version

Mathayo, Sura ya 3:

  1. Siku zile alikuja Yohana Mbatizaji akihubiri katika nyika ya Uyahudi.
  2. akisema, Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.
  3. Kwa maana huyo ndiye aliyenenwa na nabii Isaya, akisema, Sauti ya mtu aliaye nyikani, Itengenezeni njia ya Bwana, yanyosheni mapito yake.
  4. Naye Yohana huyo alikuwa na vazi lake la singa za ngamia, na mshipi wa ngozi kiunoni mwake; na chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwitu.
  5. Ndipo walipomwendea Yerusalemu, na Uyahudi wote, na nchi zote za kandokando ya Yordani;
  6. naye akawabatiza katika mto Yordani, wakiziungama dhambi zao.
  7. Lakini alipowaona wengi miongoni mwa Mafarisayo na Masadukayo wakiujia ubatizo wake, aliwaambia, Enyi wazao wa nyoka, ni nani aliyewaonya ninyi kuikimbia hasira itakayokuja?
  8. Basi zaeni matunda yapasayo toba;
  9. Wala msidhani ya kusema mioyoni mwenu, Tunaye Abrahamu ndiye baba yetu;
  10. Na sasa shoka limekwisha kuwekwa penye mashina ya miti, kwa hiyo kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni.
  11. Hakika mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba. lakini yeye ajaye nyuma yangu ana nguvu kuliko mimi, ambaye mimi sistahili hata kubeba viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto;
  12. Ambaye pepeto lake li mkononi mwake, naye atausafisha uwanda wake, na kukusanya ngano yake ghalani; bali makapi atayateketeza kwa moto usiozimika.
  13. Kisha Yesu akaja kutoka Galilaya mpaka Yordani kwa Yohana ili abatizwe naye.
  14. Lakini Yohana alitaka kumzuia akisema, Mimi nahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu?
  15. Yesu akajibu akamwambia, Acha iwe hivi sasa, kwa maana ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote. Kisha akamruhusu.
  16. Naye Yesu alipokwisha kubatizwa mara akapanda kutoka majini; na tazama, mbingu zikamfunukia, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama njiwa, akija juu yake.
  17. Na tazama, sauti kutoka mbinguni ikisema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye.