Biblia ya King James Version
Mathayo, Sura ya 24:
- Yesu akatoka nje, akaenda zake hekaluni; wanafunzi wake wakamwendea ili kumwonyesha majengo ya hekalu.
- Yesu akawaambia, Hamyaoni haya yote? Amin, nawaambia, halitasalia hapa jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomoshwa.
- Hata alipokuwa ameketi katika mlima wa Mizeituni, wanafunzi wake wakamwendea kwa faragha, wakasema, Tuambie, mambo haya yatakuwa lini? na ni nini dalili ya kuja kwako, na ya mwisho wa dunia?
- Yesu akajibu, akawaambia, Angalieni mtu asiwadanganye.
- Kwa maana wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ndiye Kristo; na watawadanganya wengi.
- Nanyi mtasikia habari za vita na fununu za vita, angalieni, msitishwe, kwa maana hayo hayana budi kutukia, lakini ule mwisho bado.
- Kwa maana taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme; kutakuwa na njaa, na tauni, na matetemeko ya nchi mahali mahali.
- Hayo yote ni mwanzo wa huzuni.
- Ndipo watawasaliti ninyi mpate dhiki, na kuwaua; nanyi mtakuwa watu wa kuchukiwa na mataifa yote kwa ajili ya jina langu.
- Ndipo wengi watakapojikwaa, na kusalitiana, na kuchukiana.
- Na manabii wengi wa uongo watatokea na kudanganya wengi.
- Na kwa sababu ya kuongezeka maasi, upendo wa wengi utapoa.
- Lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka.
- Tena habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja.
- Basi hapo mtakapoliona chukizo la uharibifu, lililonenwa na nabii Danieli, limesimama katika patakatifu, (asomaye na afahamu;)
- Ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani;
- Yeye aliye juu ya paa la nyumba asishuke kuchukua kitu nyumbani mwake;
- wala aliye shambani asirudi nyuma kuchukua nguo zake.
- Na ole wao wenye mimba na wanyonyeshao siku hizo!
- Ombeni ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi, wala siku ya sabato;
- Kwa maana wakati huo kutakuwa na dhiki kubwa, ambayo haijatokea namna yake tangu mwanzo wa ulimwengu hadi sasa, wala haitakuwapo kamwe.
- Na kama siku hizo zisingalifupizwa, asingeokoka mtu awaye yote;
- Wakati huo mtu akiwaambia, Tazama, Kristo yuko hapa, au yuko kule; usiamini.
- Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule.
- Tazama, nimekwisha kuwaambia.
- Kwa hiyo wakiwaambia, Tazama, yuko nyikani; msitoke nje; tazama, yumo katika vyumba vya siri; usiamini.
- Kwa maana kama vile umeme utokeavyo mashariki na kumulika hata magharibi; ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu.
- Kwa maana popote ulipo mzoga, ndipo watakapokusanyika tai.
- Mara baada ya dhiki ya siku hizo jua litatiwa giza, na mwezi hautatoa mwanga wake, na nyota zitaanguka kutoka mbinguni, na nguvu za mbingu zitatikisika.
- Ndipo itakapoonekana ishara ya Mwana wa Adamu mbinguni;
- Naye atawatuma malaika zake pamoja na sauti kuu ya tarumbeta, nao watawakusanya wateule wake kutoka pepo nne, toka mwisho huu wa mbingu hata mwisho huu.
- Basi kwa mtini jifunzeni mfano; tawi lake likiisha kuchipuka na kuchanua majani, mnajua kwamba wakati wa kiangazi umekaribia.
- Vivyo hivyo nanyi, myaonapo hayo yote, tambueni ya kuwa yu karibu, milangoni.
- Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatimie.
- Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.
- Lakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, hata Baba yangu peke yake.
- Lakini kama vile siku za Nuhu, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu.
- Kwa maana kama katika siku zile zilizokuwa kabla ya gharika, watu walivyokuwa wakila na kunywa, wakioa na kuolewa, hata siku ile Nuhu alipoingia katika safina;
- Na hawakujua hata gharika ikaja, ikawachukua wote; ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu.
- Ndipo wawili watakuwa shambani; mmoja atatwaliwa, na mwingine ataachwa.
- Wanawake wawili watakuwa wakisaga; mmoja atatwaliwa, na mwingine ataachwa.
- Kesheni basi, kwa maana hamjui ni saa ipi atakayokuja Bwana wenu.
- Lakini fahamuni neno hili, ya kwamba kama mwenye nyumba angalijua ni saa ngapi mwizi atakuja, angalikesha, wala asingaliiacha nyumba yake kuvunjwa.
- Kwa hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari, kwa maana katika saa msiyodhani Mwana wa Adamu yuaja.
- Ni nani basi mtumwa mwaminifu mwenye akili, ambaye bwana wake alimweka juu ya nyumba yake, awape watu chakula kwa wakati wake?
- Heri mtumwa yule ambaye bwana wake ajapo atamkuta akifanya hivyo.
- Amin, nawaambia, atamweka juu ya mali yake yote.
- Lakini mtumwa yule mbaya akisema moyoni mwake, Bwana wangu anakawia kuja;
- akaanza kuwapiga wajoli wake, na kula na kunywa pamoja na walevi;
- Bwana wa mtumwa huyo atakuja siku asiyomtazamia, na saa asiyoijua;
- Naye atamkata vipande vipande, na kumwekea fungu lake pamoja na wanafiki; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.