Biblia ya King James Version
Mathayo, Sura ya 13:
- Siku hiyohiyo Yesu alitoka nyumbani, akaketi kando ya bahari.
- Makutano makubwa yakamkusanyikia, hata akapanda chomboni, akaketi; na mkutano wote ukasimama ufuoni.
- Akawaambia mambo mengi kwa mifano, akisema, Tazama, mpanzi alitoka kwenda kupanda;
- Naye alipokuwa akipanda, mbegu nyingine zilianguka kando ya njia, ndege wakaja wakazila.
- Nyingine zilianguka penye miamba, pasipokuwa na udongo mwingi;
- Na jua lilipochomoza ziliungua; na kwa sababu hawakuwa na mizizi, zikanyauka.
- Nyingine zilianguka penye miiba; ile miiba ikamea na kuzisonga.
- Nyingine zikaanguka penye udongo mzuri, zikazaa, moja mia, moja sitini, moja thelathini.
- Mwenye masikio na asikie.
- Wanafunzi wakamwendea, wakamwambia, Mbona wasema nao kwa mifano?
- Akajibu, akawaambia, Ninyi mmejaliwa kuzijua siri za ufalme wa mbinguni, lakini wao hawakujaliwa.
- Kwa maana aliye na kitu atapewa, naye atazidishiwa tele;
- Kwa hiyo nasema nao kwa mifano, kwa sababu wanaona hawaoni; na wakisikia hawasikii, wala hawaelewi.
- Na neno la nabii Isaya linatimia kwao, likisema, Kusikia mtasikia, wala hamtaelewa; na kutazama mtatazama, wala hamtaona;
- Kwa maana mioyo ya watu hawa imekuwa mizito, na kwa masikio yao hawasikii vema, na macho yao wameyafumba; wasije wakaona kwa macho yao, na kusikia kwa masikio yao, na kufahamu kwa mioyo yao, na kuongoka, nami nikawaponya.
- Lakini macho yenu yamebarikiwa, kwa kuwa yanaona; na masikio yenu, kwa kuwa yanasikia.
- Kwa maana, amin, nawaambia, manabii wengi na watu wema walitamani kuona mnayoyaona ninyi wasiyaone; na kuyasikia mnayoyasikia, lakini hamkuyasikia.
- Basi sikilizeni mfano wa mpanzi.
- Kila mtu alisikiapo neno la ufalme asielewe nalo, huja yule mwovu na kulinyakua lililopandwa moyoni mwake. Huyu ndiye aliyepandwa kando ya njia.
- Lakini yeye aliyepandwa penye miamba, huyo ndiye alisikiaye lile neno, na kulipokea mara kwa furaha;
- lakini hana mizizi ndani yake, bali hudumu kwa muda;
- Naye aliyepandwa penye miiba ndiye alisikiaye lile neno; na shughuli za dunia na udanganyifu wa mali hulisonga lile neno, likawa halizai.
- Lakini aliyepandwa penye udongo mzuri, huyo ndiye alisikiaye lile neno na kuelewa nalo; naye huzaa matunda, huyu mia, na huyu sitini, na huyu thelathini.
- Akawatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika shamba lake;
- Lakini watu wakiwa wamelala, adui yake akaja akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake.
- Lakini jani lilipomea na kuzaa, magugu pia yakaonekana.
- Basi watumishi wa mwenye nyumba wakamwendea, wakamwambia, Bwana, hukupanda mbegu nzuri katika shamba lako? Imetoka wapi basi magugu?
- Akawaambia, Adui ndiye aliyefanya hivi. Watumwa wakamwambia, basi wataka twende tukakusanye?
- Lakini akasema, La; msije mkakusanya magugu, mkang’oa na ngano pamoja nayo.
- Viacheni vyote viwili vikue pamoja mpaka wakati wa mavuno, na wakati wa mavuno nitawaambia wavunaji, Yakusanyeni kwanza magugu, mkayafunge matita matita mkayachome;
- Akawatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na punje ya haradali aliyoitwaa mtu, akaipanda katika shamba lake;
- ambayo ni ndogo kuliko mbegu zote, lakini ikiisha kumea huwa kubwa kuliko mboga zote, ikawa mti, hata ndege wa angani huja na kukaa katika matawi yake.
- Akawaambia mfano mwingine; Ufalme wa mbinguni umefanana na chachu aliyotwaa mwanamke, akaificha ndani ya pishi tatu za unga, hata ukachacha wote.
- Hayo yote Yesu aliwaambia makutano kwa mifano; wala pasipo mfano hakusema nao;
- ili litimie neno lililonenwa na nabii, akisema, Nitafumbua kinywa changu kwa mifano; Nitayatamka mambo yaliyofichwa tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu.
- Yesu akawaaga makutano, akaingia nyumbani; wanafunzi wake wakamwendea, wakasema, Tufafanulie mfano wa magugu ya shambani.
- Akajibu, akawaambia, Apandaye mbegu njema ni Mwana wa Adamu;
- Shamba ni ulimwengu; mbegu njema ni wana wa ufalme; bali magugu ni wana wa yule mwovu;
- Adui aliyeyapanda ni Ibilisi; mavuno ni mwisho wa dunia; na wavunaji ni malaika.
- Basi kama vile magugu yakusanywavyo na kuchomwa motoni; ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia hii.
- Mwana wa Adamu atawatuma malaika zake, nao watakusanya kutoka katika ufalme wake machukizo yote, na watenda maovu;
- na kuwatupa katika tanuru ya moto, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.
- Ndipo wenye haki watakapong’aa kama jua katika ufalme wa Baba yao. Mwenye masikio na asikie.
- Tena ufalme wa mbinguni umefanana na hazina iliyositirika katika shamba; ambayo mtu akiipata huificha, na kwa furaha yake akaenda akauza alivyo navyo vyote, na kulinunua shamba lile.
- Tena ufalme wa mbinguni umefanana na mfanyabiashara, mwenye kutafuta lulu nzuri;
- Naye alipopata lulu moja ya thamani kubwa, akaenda akauza alivyo navyo vyote, akainunua.
- Tena ufalme wa mbinguni umefanana na wavu uliotupwa baharini, ukakusanya kila aina;
- Ulipojaa waliuvuta ufuoni, wakaketi, wakakusanya walio wema vyomboni, lakini wabaya wakawatupa.
- Ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia; malaika watatokea, watawatenga waovu mbali na wenye haki;
- na kuwatupa katika tanuru ya moto; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.
- Yesu akawaambia, Mmeelewa haya yote? Wakamwambia, Naam, Bwana.
- Kisha akawaambia, “Kwa hiyo, kila mwalimu wa Sheria aliyefundishwa kuhusu Ufalme wa mbinguni amefanana na mtu mwenye nyumba atoaye katika hazina yake vitu vipya na vya kale.”
- Ikawa Yesu alipomaliza mifano hiyo, alitoka huko.
- Hata alipofika nchi ya kwao, akawafundisha katika sinagogi lao, hata wakashangaa, wakasema, Huyu amepata wapi hekima hii na miujiza hii?
- Huyu si mwana wa seremala? mama yake si anaitwa Mariamu? na ndugu zake Yakobo, na Yose, na Simoni, na Yuda?
- Na dada zake, je, hawako pamoja nasi wote? Basi, huyu ameyapata wapi mambo haya yote?
- Nao wakachukizwa naye. Lakini Yesu akawaambia, Nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake na nyumbani mwake.
- Wala hakufanya miujiza mingi huko kwa sababu ya kutokuamini kwao.