Biblia ya King James Version
Mathayo, Sura ya 12:
- Wakati huo Yesu alipitia katika mashamba siku ya sabato; Wanafunzi wake walikuwa na njaa, wakaanza kuvunja masuke na kula.
- Mafarisayo walipoona, wakamwambia, Tazama, wanafunzi wako wanafanya jambo ambalo si halali siku ya Sabato.
- Lakini akawaambia, Hamkusoma alivyofanya Daudi alipokuwa na njaa, yeye na wale waliokuwa pamoja naye;
- Jinsi alivyoingia katika nyumba ya Mungu, akaila ile mikate ya wonyesho, ambayo haikuwa halali kwake kuila, wala kwa wale waliokuwa pamoja naye, ila kwa makuhani peke yao?
- Au hamjasoma katika torati ya kwamba siku ya sabato makuhani hekaluni huinajisi sabato wala hawana lawama?
- Lakini nawaambieni, aliye mkuu kuliko Hekalu yuko hapa.
- Lakini kama mngejua maana ya maneno haya, Nataka rehema, wala si dhabihu, msingaliwahukumu wasio na hatia.
- Kwa maana Mwana wa Adamu ndiye Bwana hata wa siku ya sabato.
- Naye alipotoka huko aliingia katika sinagogi lao;
- Na tazama, palikuwa na mtu mwenye mkono uliopooza. Wakamwuliza, wakisema, Je! ni halali kuponya mtu siku ya sabato? ili wapate kumshtaki.
- Akawaambia, Ni mtu yupi kwenu mwenye kondoo mmoja, na ikiwa ataanguka shimoni siku ya sabato, hatamshika na kumtoa?
- Je! mtu ni bora kuliko kondoo? Kwa hiyo ni halali kutenda mema siku ya sabato.
- Kisha akamwambia yule mtu, Nyosha mkono wako. Naye akaunyosha; ukawa mzima kama ule mwingine.
- Basi Mafarisayo wakatoka nje, wakafanya shauri juu yake jinsi ya kumwangamiza.
- Naye Yesu alipojua hayo, aliondoka hapo; na makutano mengi wakamfuata, akawaponya wote;
- Akawaonya wasimjulishe.
- ili litimie neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema,
- Tazama mtumishi wangu niliyemchagua; mpendwa wangu, ambaye nafsi yangu imependezwa naye, nitaweka roho yangu juu yake, naye atawahubiri mataifa hukumu.
- Hatashindana, wala hatalia; wala hakuna mtu atakayesikia sauti yake katika njia kuu.
- Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi utokao moshi hatauzima, hata atakapoileta hukumu iwe ya ushindi.
- Na katika jina lake mataifa watalitumainia.
- Kisha akaletwa kwake mtu mwenye pepo, kipofu, naye ni bubu;
- Watu wote wakashangaa, wakasema, Huyu siye Mwana wa Daudi?
- Lakini Mafarisayo waliposikia, walisema, Mtu huyu hatoi pepo, ila kwa Beelzebuli mkuu wa pepo.
- Naye Yesu akayajua mawazo yao, akawaambia, Kila ufalme ukifitinika juu ya nafsi yake, hufanyika ukiwa; na kila mji au nyumba iliyofitinika juu ya nafsi yake haitasimama;
- Na kama Shetani akitoa Shetani, amegawanyika juu yake mwenyewe; basi ufalme wake utasimamaje?
- Na mimi nikitoa pepo kwa Beelzebuli, watoto wenu huwatoa kwa nani? kwa hiyo watakuwa waamuzi wenu.
- Lakini ikiwa mimi ninatoa pepo kwa Roho wa Mungu, basi Ufalme wa Mungu umewajia.
- Au mtu awezaje kuingia ndani ya nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuteka mali yake, isipokuwa kwanza amfunge yule mwenye nguvu? ndipo atakapoiteka nyumba yake.
- Yeye asiye pamoja nami yu kinyume changu; na asiyekusanya pamoja nami hutawanya.
- Kwa sababu hiyo nawaambia, Kila dhambi na kufuru watasamehewa wanadamu, lakini kufuru dhidi ya Roho Mtakatifu hawatasamehewa.
- Na mtu ye yote atakayenena neno juu ya Mwana wa Adamu atasamehewa, bali yeye atakayenena neno juu ya Roho Mtakatifu hatasamehewa katika ulimwengu huu, wala katika ule ujao.
- Ufanyeni mti kuwa mzuri na matunda yake kuwa mazuri; au ufanyeni mti kuwa mbaya na matunda yake mabaya, kwa maana kwa matunda yake mti hutambulikana.
- Enyi wazao wa nyoka, mwawezaje kunena mema, mkiwa waovu? maana kinywa cha mtu hunena yauujazayo moyo.
- Mtu mwema katika hazina njema ya moyo wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya moyo wake hutoa yaliyo maovu.
- Lakini nawaambieni, kila neno lisilo maana watakalolinena wanadamu, watatoa hesabu ya neno hilo siku ya hukumu.
- Kwa maana kwa maneno yako utahesabiwa haki, na kwa maneno yako utahukumiwa.
- Kisha baadhi ya walimu wa Sheria na Mafarisayo wakamjibu, “Mwalimu, tunataka kuona ishara kutoka kwako.”
- Akajibu, akawaambia, Kizazi kibaya na cha zinaa chatafuta ishara; wala halitapewa ishara, ila ishara ya nabii Yona.
- Maana kama vile Yona alivyokuwa siku tatu mchana na usiku ndani ya tumbo la nyangumi huyo; vivyo hivyo Mwana wa Adamu atakuwa siku tatu mchana na usiku katika moyo wa nchi.
- Watu wa Ninawi watasimama katika hukumu pamoja na kizazi hiki, nao watakihukumu; kwa sababu walitubu kwa mahubiri ya Yona; na tazama, mkuu kuliko Yona yuko hapa.
- Malkia wa kusini atasimama siku ya hukumu pamoja na kizazi hiki, naye atakihukumu kuwa kina hatia; na tazama, aliye mkuu kuliko Sulemani yuko hapa.
- Pepo mchafu akimtoka mtu, hupitia mahali pasipo maji akitafuta mahali pa kupumzika, asipate.
- Ndipo husema, Nitarudi nyumbani kwangu nilikotoka; na ajapo anaikuta tupu, imefagiwa na kupambwa.
- Kisha huenda akawachukua pamoja naye pepo wengine saba waovu kuliko yeye mwenyewe, nao huingia na kukaa humo. Ndivyo itakavyokuwa kwa kizazi hiki kiovu.
- Alipokuwa bado anazungumza na umati wa watu, mama yake na ndugu zake walisimama nje, wakitaka kusema naye.
- Mtu mmoja akamwambia, Tazama, mama yako na ndugu zako wamesimama nje, wanataka kusema nawe.
- Akajibu, akamwambia yule aliyemwambia, Mama yangu ni nani? na ndugu zangu ni akina nani?
- Akaunyosha mkono wake kuelekea wanafunzi wake, akasema, Tazama, mama yangu na ndugu zangu!
- Kwa maana yeyote anayefanya mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni, huyo ndiye kaka yangu, dada yangu na mama yangu.