Biblia ya King James Version
Mathayo, Sura ya 11:
- Ikawa Yesu alipomaliza kuwaagiza wanafunzi wake kumi na wawili, alitoka huko kwenda kufundisha na kuhubiri katika miji yao.
- Yohana aliposikia kule gerezani matendo ya Kristo, aliwatuma wawili wa wanafunzi wake.
- wakamwambia, Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine?
- Yesu akajibu, akawaambia, Nendeni mkamwambie Yohana tena yale mnayoyasikia na kuyaona;
- Vipofu wanaona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, na maskini wanahubiriwa Habari Njema.
- Na heri mtu ye yote asiyechukizwa kwa ajili yangu.
- Na hao walipokuwa wakienda, Yesu alianza kuwaambia makutano habari za Yohana, Mlitoka kwenda nyikani kuona nini? Mwanzi unaotikiswa na upepo?
- Lakini mlitoka kwenda kuona nini? Mtu aliyevaa mavazi laini? tazama, wavaao nguo laini wamo katika nyumba za wafalme.
- Lakini mlitoka kwenda kuona nini? Nabii? naam, nawaambia, na zaidi ya nabii.
- Kwa maana huyu ndiye aliyeandikiwa, Tazama, namtuma mjumbe wangu mbele ya uso wako, atakayeitengeneza njia yako mbele yako.
- Amin, nawaambia, Hajaondokea mtu katika wale waliozaliwa na wanawake aliye mkuu kuliko Yohana Mbatizaji; walakini aliye mdogo katika ufalme wa mbinguni ni mkuu kuliko yeye.
- Na tangu siku za Yohana Mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu wauteka.
- Kwa maana manabii wote na torati walitabiri mpaka Yohana.
- Na kama mnataka kupokea, huyo ndiye Eliya ambaye angekuja.
- Mwenye masikio na asikie.
- Lakini nitakifananisha na nini kizazi hiki? Ni kama watoto wanaokaa sokoni na kuwaita wenzao.
- wakisema, Tuliwapigia filimbi, wala hamkucheza; tumeomboleza kwenu, wala hamkuomboleza.
- Kwa maana Yohana alikuja hali wala hanywi, wakasema, Ana pepo.
- Mwana wa Adamu alikuja, anakula na kunywa, wakasema, Tazama, mtu mlafi na mlevi, rafiki yao watoza ushuru na wenye dhambi. Lakini hekima inahesabiwa haki kwa watoto wake.
- Ndipo akaanza kuikemea miji ambayo ndani yake ilifanyika miujiza yake mingi, kwa sababu haikutubu.
- Ole wako Korazini! Ole wako, Bethsaida! kwa maana kama miujiza iliyofanyika kwenu ingalifanyika katika Tiro na Sidoni, wangalitubu zamani zao wakiwa wamevaa magunia na majivu.
- Lakini nawaambieni, itakuwa rahisi Tiro na Sidoni kustahimili adhabu yake siku ya hukumu kuliko ninyi.
- Na wewe, Kapernaumu, uliyeinuliwa hata mbinguni, utashushwa hata kuzimu;
- Lakini nawaambieni, itakuwa rahisi nchi ya Sodoma kustahimili adhabu yake siku ya hukumu kuliko wewe.
- Wakati huo Yesu akajibu, akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga.
- Vivyo hivyo, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyopendeza machoni pako.
- Nimekabidhiwa vyote na Baba yangu, wala hakuna amjuaye Mwana, ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba, ila Mwana, na ye yote ambaye Mwana apenda kumfunulia.
- Njooni kwangu ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.
- Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu.
- Kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.