Biblia ya King James Version
Marko, Sura ya 2:
- Akaingia tena Kapernaumu baada ya siku kadha wa kadha; na ikasikika kwamba yumo nyumbani.
- Mara watu wengi wakakusanyika, hata nafasi ya kuwapokea ikakosa, hata mlangoni, naye akawahubiria lile neno.
- Wakaja kwake mtu mmoja mwenye kupooza, anachukuliwa na watu wanne.
- Na walipokuwa hawawezi kumkaribia kwa sababu ya umati wa watu, wakaitoboa dari pale alipokuwa;
- Yesu alipoiona imani yao, akamwambia yule mwenye kupooza, Mwanangu, umesamehewa dhambi zako.
- Lakini baadhi ya waandishi walikuwa wameketi, wakifikiri mioyoni mwao,
- Kwa nini mtu huyu anakufuru hivi? ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa Mungu peke yake?
- Mara Yesu akatambua katika roho yake ya kuwa wanafikiri hivyo mioyoni mwao, akawaambia, Mbona mnafikiri mambo haya mioyoni mwenu?
- Ni lipi lililo rahisi zaidi kumwambia mwenye kupooza, Umesamehewa dhambi zako; au kusema, Ondoka, ujitwike godoro lako, uende?
- Lakini mpate kujua ya kuwa Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (akamwambia yule mwenye kupooza),
- Nakuambia, Ondoka, ujitwike godoro lako, uende zako nyumbani kwako.
- Mara akainuka, akajitwika godoro, akaenda mbele yao wote; hata wakastaajabu wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, namna hii hatujapata kuiona kamwe.
- Akatoka tena kando ya bahari; umati wote ukamwendea, naye akawafundisha.
- Naye alipokuwa akipita akamwona Lawi mwana wa Alfayo ameketi ofisini, akamwambia, Nifuate. Akainuka, akamfuata.
- Ikawa Yesu alipokuwa ameketi kula chakula nyumbani mwake, watoza ushuru wengi na wenye dhambi walikuwa wameketi pamoja na Yesu na wanafunzi wake; kwa maana walikuwa wengi wakamfuata.
- Waandishi na Mafarisayo walipomwona akila pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi, wakawaambia wanafunzi wake, Mbona anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi?
- Yesu aliposikia akawaambia, Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi. Sikuja kuwaita watu wema, bali wenye dhambi.
- Wanafunzi wa Yohana na wa Mafarisayo walikuwa na desturi ya kufunga; wakaja na kumwambia, Mbona wanafunzi wa Yohana na wa Mafarisayo hufunga, lakini wanafunzi wako hawafungi?
- Yesu akawaambia, Je! maadamu wana bwana-arusi pamoja nao hawawezi kufunga.
- Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana-arusi, ndipo watakapofunga siku zile.
- Hakuna mtu ashonaye kiraka cha nguo mpya katika vazi kuukuu;
- Wala hakuna mtu atiaye divai mpya katika viriba vikuukuu;
- Ikawa siku ya sabato alipita katika mashamba ya ngano; wanafunzi wake wakaanza kwenda kukwanyua masuke.
- Mafarisayo wakamwambia, Tazama, mbona wanafanya jambo lisilo halali siku ya sabato?
- Akawaambia, Hamkusoma alivyofanya Daudi, alipokuwa na njaa, yeye na wale waliokuwa pamoja naye?
- Jinsi alivyoingia katika nyumba ya Mungu siku za Abiathari, kuhani mkuu, akaila ile mikate ya wonyesho, ambayo hairuhusiwi kuliwa ila makuhani, akawapa na wale waliokuwa pamoja naye?
- Akawaambia, Sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu, si mwanadamu kwa ajili ya sabato;
- Kwa hiyo Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato pia.