Kitabu cha Kwanza cha Yohana, Biblia ya Sauti Bila Malipo, Biblia ya King James Version katika Kiswahili

Biblia ya King James Version

Yohana wa 1, Sura ya 1:

  1. Lile lililokuwako tangu mwanzo, tulilolisikia, tuliloliona kwa macho yetu, tulilolitazama, na mikono yetu kulishika, la Neno la uzima;
  2. (Kwa maana uzima huo ulidhihirika, nasi tumeuona, na twashuhudia na kuwapasha habari ule uzima wa milele, uliokuwa kwa Baba, ukadhihirishwa kwetu;)
  3. Hilo tuliloliona na kulisikia twawahubiri ninyi, ili nanyi pia mpate kushirikiana nasi; na ushirika wetu ni pamoja na Baba, na pamoja na Mwanawe Yesu Kristo.
  4. Tunawaandikia ninyi mambo haya ili furaha yenu ikamilike.
  5. Basi, hii ndiyo habari tuliyoisikia kwake, na kuihubiri kwenu, ya kwamba Mungu ni nuru, wala hamna giza lolote ndani yake.
  6. Tukisema ya kwamba tuna ushirika naye, na tukienenda gizani, twasema uongo, wala hatuifanyi iliyo kweli;
  7. Lakini tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake Yesu Kristo, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote.
  8. Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu.
  9. Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.
  10. Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya yeye kuwa mwongo, wala neno lake halimo mwetu.