Biblia ya King James Version
Yohana wa 1, Sura ya 1:
- Lile lililokuwako tangu mwanzo, tulilolisikia, tuliloliona kwa macho yetu, tulilolitazama, na mikono yetu kulishika, la Neno la uzima;
- (Kwa maana uzima huo ulidhihirika, nasi tumeuona, na twashuhudia na kuwapasha habari ule uzima wa milele, uliokuwa kwa Baba, ukadhihirishwa kwetu;)
- Hilo tuliloliona na kulisikia twawahubiri ninyi, ili nanyi pia mpate kushirikiana nasi; na ushirika wetu ni pamoja na Baba, na pamoja na Mwanawe Yesu Kristo.
- Tunawaandikia ninyi mambo haya ili furaha yenu ikamilike.
- Basi, hii ndiyo habari tuliyoisikia kwake, na kuihubiri kwenu, ya kwamba Mungu ni nuru, wala hamna giza lolote ndani yake.
- Tukisema ya kwamba tuna ushirika naye, na tukienenda gizani, twasema uongo, wala hatuifanyi iliyo kweli;
- Lakini tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake Yesu Kristo, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote.
- Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu.
- Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.
- Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya yeye kuwa mwongo, wala neno lake halimo mwetu.