Biblia ya King James Version

1 Wakorintho, Sura ya 2:

  1. Nami, ndugu zangu, nilipokuja kwenu, sikuja kwa ufasaha wa usemi, wala wa hekima, niwahubiri ushuhuda wa Mungu.
  2. Kwa maana naliazimu nisijue neno lo lote kwenu ila Yesu Kristo, naye amesulubiwa.
  3. Nami nalikuwa kwenu katika udhaifu na woga na matetemeko mengi.
  4. Na neno langu na kuhubiri kwangu hakukuwa kwa maneno ya hekima yenye kuvutia akili ya watu, bali kwa dalili za Roho na za nguvu.
  5. Ili imani yenu isiwe katika hekima ya wanadamu, bali katika nguvu za Mungu.
  6. Lakini twanena hekima miongoni mwao walio wakamilifu;
  7. Bali twanena hekima ya Mungu katika siri, ile hekima iliyofichwa, ambayo Mungu aliiazimu tangu milele kwa utukufu wetu;
  8. Jambo ambalo wakuu wa dunia hii hawakulifahamu; kwa maana kama wangalilijua, wasingalimsulubisha Bwana wa utukufu.
  9. Lakini kama ilivyoandikwa, Mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia, wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu, mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao.
  10. Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho wake, maana Roho huchunguza yote, naam, mafumbo ya Mungu.
  11. Kwa maana ni nani ajuaye mambo ya mwanadamu isipokuwa roho ya mwanadamu iliyo ndani yake? Vivyo hivyo na mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu.
  12. Sisi hatukuipokea roho ya dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu; ili tupate kuyajua tuliyokirimiwa na Mungu.
  13. Nayo twayanena, si kwa maneno yanayofundishwa kwa hekima ya wanadamu, bali yanayofundishwa na Roho; tukilinganisha mambo ya rohoni na ya rohoni.
  14. Lakini mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu, maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa sababu yatambulikana kwa jinsi ya rohoni.
  15. Lakini mtu wa rohoni huyatambua yote, wala yeye hatambuliwi na mtu.
  16. Maana ni nani aliyeijua nia ya Bwana, apate kumfundisha? Lakini sisi tunayo nia ya Kristo.