Biblia ya King James Version
1 Timotheo, Sura ya 2:
- Basi, kabla ya mambo yote, nataka dua, na sala, na maombezi, na shukrani, zifanyike kwa ajili ya watu wote;
- Kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka; ili tuishi maisha ya utulivu na amani, katika utauwa wote na ustahivu.
- Kwa maana hili ni jema na lakubalika mbele za Mungu Mwokozi wetu;
- ambaye anataka watu wote waokolewe, na kupata kujua yaliyo kweli.
- Kwa maana kuna Mungu mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu;
- ambaye alijitoa mwenyewe kuwa ukombozi kwa ajili ya wote, utakaoshuhudiwa kwa wakati wake.
- Nami naliwekwa niwe mhubiri na mtume, (nasema kweli katika Kristo, wala sisemi uongo) mwalimu wa watu wa mataifa katika imani na kweli.
- Basi, nataka wanaume wasali kila mahali, huku wakiinua mikono iliyotakata pasipo hasira na shaka.
- Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa mavazi ya thamani;
- Bali kwa matendo mema, iwapasavyo wanawake wanaokiri kuwa wanamcha Mungu.
- Mwanamke na ajifunze katika ukimya kwa utiifu wote.
- Lakini simruhusu mwanamke kufundisha, wala kumtawala mwanamume, bali awe kimya.
- Kwa maana Adamu ndiye aliyeumbwa kwanza, kisha Hawa.
- Wala Adamu hakudanganywa, bali mwanamke alidanganywa akawa katika hali ya kukosa.
- Walakini ataokolewa kwa uzazi, ikiwa watadumu katika imani na upendo na utakatifu pamoja na kiasi.